BOOMPLAY KUSHIRIKIANA KIBIASHARA NA WARNER MUSIC GROUP

0
YIKA BOY MEDIA
Boom Play

DAR ES SALAAM, TANZANIA – Boomplay ni app inayotoa huduma ya
kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika, imesaini makubaliano ya
kushirikiana kibiashara na Warner Music, kwa lengo la kuongeza wigo wa
upatikanaji wa kazi za muziki wa kampuni hiyo maeneo mengi zaidi
duniani.

Moja kati ya makubaliano hayo ni pamoja na kuipa fursa Boomplay,
kusambaza kazi za muziki zaidi ya milioni moja kutoka Warner Music
kwenda kwa watumiaji wake nchini Tanzania na mataifa mengine tisa ya
kiafrika ikiwemo Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Kenya, Nigeria, Rwanda,
Senegal, Uganda na Zambia.

Ushirikiano huu pia utawawezesha wasanii wa Warner Music kujitangaza
zaidi na tena kwa haraka mbele ya mamilioni ya watumiaji wa Boomplay na
kuiwezesha app hiyo ya kijanja kuifikia dhamira yake ya kukusanya kazi
za muziki kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kuzileta barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Boomplay, Bwana Joe He, amesema, “Makubaliano
haya na makampuni makubwa ya muziki ya kimataifa kama Warner Music,
yanatuwezesha sisi kuyakaribia mafanikio ya malengo yetu ya kujenga
jukwaa kubwa la muziki linaloaminika na wengi barani Afrika”

“Tunataka kila mpenda muziki awe na uwezo wa kupata nyimbo na video,
wakati wowote na mahali popote. Tunatarajia uwepo wa mafanikio bora
kupitia ushirikiano huu na muendelezo mzuri wa kibiasha tukiwa na Warner
Music hasa katika kipindi hiki kizuri kwenye fani ya muziki Afrika”
aliongeza Bwana He.

Pia, Meneja wa Boomplay Tanzania, Bi Natasha Stambuli amesema,
“Tunatarajia mafanikio makubwa na fursa mbalimbali yakiwa ni matokeo ya
makubaliano kama haya katika tasnia ya muziki nchini Tanzania. Huu ni
mwanzo wa mambo makubwa zaidi hapo mbeleni kwa Boomplay pamoja na Warner
Music.”

Naye Alfonso Perez Soto, ambaye ni Makamu wa rais wa Warner Music
huko Ulaya Mashariki, Mashariki ya Kati na Afrika amebainisha kwamba
“Tuna furaha kushirikiana na Boomplay kuleta kazi kutoka kwa wasanii
wetu kwa mamilioni ya wasikiliza na wapenzi wa muziki barani Afrika.
Boomplay tayari imewafikia watu wengi barani Afrika huku wakiendelea
kupanua wigo. Hii ni fursa kubwa kwa wasanii wetu kupata mashabiki wengi
zaidi.”

“Ningependa kuwashukuru, Charlie White, Marc Latilla na Reni Adadevoh
kutoka Warner Music kwa mchango wao mkubwa kusaidia kufanikisha
makubaliano haya” aliongeza Bwana Soto.

Toka mwaka uliopita, Boomplay imeendelea kutikisa anga la muziki kwa
kutangaza ushirikiano na makampuni mbali mbali makubwa ili kupata
watumiaji wengi zaidi kila mwezi na kutoa version (toleo) ya iOS mwezi
Disemba mwaka 2018.

Pamoja na uwepo wa lebo kubwa za muziki zinazojiunga na Boomplay, app
hii imejidhatiti kwa kujenga na kuboresha nafasi yake barani Afrika.
Boomplay, ambayo mpaka kufikia mwezi Februari, 2019, ilijikusanyia zaidi
ya watumiaji milioni 42, ina kazi za muziki zaidi ya nyimbo milioni 5,
na maelfu ya video kutoka kwa wasanii wa Tanzania na wa kimataifa.

Kuhusu Boomplay

Boomplay (ambayo awali ilikuwa ikifahamika kama Boomplayer), ni
jukwaa linalotoa huduma ya kusikiliza na kupakua (download) muziki
ambayo ipo chini ya umiliki wa kampuni ya Transsnet Music Limited.

Malengo ya app hii ni kutengeneza jukwaa kubwa na la kutegemewa na
wasanii na wazalishaji wa muziki katika usambazaji wa  kazi hizo za
sanaa. Boomplay ilishinda tuzo ya “Application bora Africa” kwenye tuzo
za “AppsAfrica Awards” mwaka 2017.

Kwa sasa Boomplay ndio application kubwa na inayokuwa kwa kasi sana barani Afrika, ikiwa na nyimbo na video zaidi ya milioni 5.

Watumiaji wake wanaweza kusikiliza na kuangalia video bure, kwa
kujisajili (subscribe) kupitia vifurushi vya siku,wiki au vile vya mwezi
ambapo ambavyo vinawawezesha kuhifadhi (save) nyimbo offline au kununua
nyimbo. Huduma hiyo kwa sasa inapatikana Android, iOS na wavuti.